Baada ya Acacia kutangaza kupunguza operesheni zake Bulyanhulu, kampuni hiyo imeanza kuikabidhi Serikali baadhi ya mali zake kwenye Mgodi wa Buzwagi ambao unatarajiwa kufungwa miaka mitatu ijayo.
Katika utekelezaji wa makabidhiano hayo, jana kampuni hiyo iliikabidhi Serikali uwanja wa ndege uliopo katika mgodi huo. Huu ni mgodi wa pili kufungwa na kampuni hiyo baada ya ule wa Tulawaka ambao iliuuza kwa Shirika la Taifa la Madini (Stamico) mwaka 2013.
Jana, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema hiyo ni hatua ya awali katika mchakato wa mgodi huo kusitisha shughuli zake za uchimbaji madini kwa mujibu wa mkataba uliopo.
“Tumeanza na uwanja wa ndege baadaye tutakabidhiwa majengo na vitu vingine kama ulivyo utaratibu,” alisema Telack.
Alisema Desemba mwaka huu utakuwa mwisho wa shughuli za uchimbaji na baada ya hapo wataanza kusaga mawe yaliyochimbwa kwa miaka mitatu mfululizo mpaka 2020.
Juzi, kampuni hiyo ilitoa taarifa ikibainisha lengo lake la kupunguza operesheni zake kwenye Mgodi wa Bulyanhulu baada ya kuzuiwa kusafirisha mchanga wa dhahabu tangu Machi hivyo gharama za uendeshaji kuwa juu kuliko ilivyotarajia huku mapato yakishuka.
Kwa miezi sita ya kutosafirisha mchanga huo, Acacia imedai kuwa imepoteza zaidi ya Sh583 bilioni.
Katika utekelezaji wa mkakati wake wa kubana matumizi, kampuni hiyo inatarajia kupunguza wafanyakazi na kandarasi mbalimbali ilizonazo. Kwa sasa, ina wafanyakazi 1,200 na wakandarasi 800 kwenye Mgodi wa Bulyanhulu.
Taarifa hiyo pia ilibainisha kucheleweshwa kwa leseni za wakandarasi wa machimbo ya chini ya ardhi kwenye Mgodi wa Buzwagi jambo linaloongeza changamoto.
Ingawa mazungumzo baina ya Serikali na kampuni ya Barrick inayomiliki asilimia 64 ya hisa za Acacia bado yanaendelea, uamuzi wa kupunguza operesheni kwenye mgodi huo unatarajiwa kupunguza uzalishaji kwa karati 100,000 kutoka kati ya karati 850,000 hadi 900,000 zilizokadiriwa awali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu, bei ya hisa zake kwenye Soko la London (LSE) ilishuka kwa asilimia sita mpaka Pauni 1.94 huku kwenye Soko la Dar es Salaam (DSE) ikishuka kutoka Sh5,940 mpaka Sh5,400 jana mchana. Tangu kutolewa kwa zuio hilo, bei ya hisa hizo imepungua kwa asilimia 65.
Taratibu za kupunguza operesheni zake kwenye Mgodi wa Bulyanhulu zitakamilika ndani ya miezi mitatu na kampuni hiyo inaamini itatengamaa kuanzia mwakani.
No comments:
Post a Comment